THRDC YAFANYA MAFUNZO YA SIKU MBILI YA ELIMU YA SHERIA KWA WANASHERIA WA HAKI ZA BINADAMU NCHINI TANZANIA

Leo tarehe 27 Juni 2025, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Wanasheria Afrika (PALU) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia mradi wa SCATZ unaofadhiliwa na Umoja wa ulaya (EU), umeanza rasmi mafunzo ya siku mbili ya elimu ya sheria kwa wanasheria wa haki za binadamu nchini Tanzania. Mafunzo haya yanafanyika katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma.

Mafunzo haya yamewakutanisha zaidi ya wanasheria na mawakili 50 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yakiwa pamoja na wawasilishaji wa mada mbalimbali wakiwemo majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania kama Mheshimiwa Jaji Robert Makaramba na Mheshimiwa Jaji Fauz Twaibu sambamba na viongozi mbalimbali wa vyama na jumuia za wanasheria wameshiriki, akiwemo Makamu wa Rais wa TLS, Katibu wa EALS, pamoja na wawakilishi wa ZAFELA na PALU yakiwa ni utekelezaji na muendelezo wa mpango endelevu wa THRDC katika kutoa elimu endelevu ya haki za binadamu (CLE) kwa wanasheria na mawakili nchini Tanzania.

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuimarisha uwezo wa wanasheria nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa haki unaozingatia misingi ya haki za binadamu, kupitia matumizi bora ya sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa, huku wakizingatia utawala wa sheria, maadili ya taaluma, na kanuni za haki kwa wote. Mafunzo haya pia yanakusudia kuongeza ufanisi wa wanasheria katika kusimamia masuala ya haki katika jamii kwa kutumia mifumo ya kisheria na nyenzo za kimataifa za haki za binadamu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo haya, Wakili Onesmo Olengurumwa – Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, alisisitiza kuwa mafanikio katika kulinda haki za binadamu na utawala bora yanahitaji ushirikiano kati ya asasi za kiraia, jumuia/vyama vya wanasheria, na serikali jambo ambalo mradi huu wa SCATZ na kutiliwa mkazo. Aliongeza kuwa kuelekea Uchaguzi mkuu wa 2025, ni muhimu kwa wanasheria kutambua wajibu wao katika kuchambua na kushughulikia changamoto za kisheria zitakazojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Mafunzo haya pia yanatoa fursa ya kipekee kwa washiriki kujadili masuala muhimu kama vile dhana ya mashauri ya maslahi ya umma (PIL), nafasi ya jumiua/vyama vya wanasheria katika kuendeleza kesi hizo, matumizi ya mikataba ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa katika kulinda haki za wananchi, pamoja na masuala ya maadili ya wanasheria katika matumizi sahihi ya teknologia na mitandao ya kijamii kwenye dunia ya sasa ya kidijitali.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu – THRDC
27 Juni 2025

JusticeForAllPeople CLE2025
AccessToJustice EU
HumanRightsTZ
Tanganyika Law Society (TLS)
East Africa Law Society
ZAFELA Member
PALU SIDA Ford Foundation
PIA

Related Posts